Saturday 30 September 2017

Jeshi la Uganda latoa tamko kuhusu ‘mapigano’ bungeni

Jeshi la Uganda limezungumzia hatua iliyochukuliwa na vyombo vya usalama kuwaondoa kwa nguvu wabunge waliotimuliwa bungeni na Spika, Rebbeka Kagada, Jumatano wiki hii.

Akizungumzia uamuzi huo, Jenerali Elly Tumwine alisema kuwa uamuzi huo ulikuwa sahihi kwani wabunge hao walivunja sheria na kwenda kinyume na kanuni zinazowalinda ndani ya bunge hilo kwa kufanya vurugu na kupigana.

Wabunge 25 wa upinzani walisimamishwa na Spika wa Bunge hilo baada ya kupatikana na hatia ya kuhusika katika vurugu iliyosababisha vikao vya bunge kusimamishwa kwa muda. Vurugu hizo ziliibuka wakati mjadala wa kuondoa ukomo wa umri wa kugombea urais ulipowasilishwa bungeni.

Vurugu hizo zilihusisha mapigano ya ngumi, kukabana na kurushiana viti kati ya wabunge wa kambi ya upinzani na wabunge wa chama tawala kinachomuunga mkono Rais Yoweri Museveni pamoja na mawaziri wake.

Mbali na vurugu hizo ndani ya Bunge, kiongozi wa chama cha upinzani ambaye ni mpinzani mkuu wa Rais Museveni, Kizza Besigye alishikiliwa na jeshi la polisi baada ya kutaka kufanya maandamano ya kupinga muswada huo.

Kwa mujibu wa ibara ya 102 (b) ya Katiba ya nchi hiyo, ukomo wa umri wa kugombea urais ni miaka 75 tu. Hivyo, kifungu hicho kingewemzuia Rais Museveni mwenye miaka 73 kugombea urais katika awamu nyingine.
Share:

Friday 29 September 2017

Serikali yalifungia gazeti la Raia Mwema


Serikali imesitisha uchapishaji na usambazaji wa gazeti la kila wiki la Raia Mwema kwa muda wa siku 90 kuanzia leo.

Mkurugenzi wa Idara ya Habari (Maelezo) na Msemaji Mkuu wa Serikali, Dk Hassan Abbasi amesema leo Alhamisi kuwa agizo hilo pia linahusu toleo la mtandaoni.

Dk Abbasi amesema adhabu hiyo inatokana na toleo namba 529 la Septemba 27 hadi  Oktoba 3 lililochapisha habari ya uchambuzi inayosomeka “Urais utamshinda John  Magufuli.”

Mwenyekiti wa Bodi ya Raia Mwema, Jenerali Ulimwengu amesema wameambiwa sababu ya kusitishwa kwa gazeti hilo ni habari hiyo.

Ulimwengu amesema kwa sasa wanashauriana kuona ni nini cha kufanya.

Dk Abbasi amesema katika taarifa kwa vyombo vya habari kuwa, Serikali inasisitiza uchambuzi huo ni maoni ya Raia Mwema  ya haki (fair comment), hata hivyo, kwa bahati mbaya, na nia ovu, makala hiyo ilisheheni nukuu za kutunga na zisizo za kweli zikimsingizia Rais John Magufuli.

Amesema gazeti hilo pia limewahi kuonywa kwa makosa mbalimbali.

Amesema nukuu za uongo, kutungwa na zenye nia mbaya zikidai Rais alipata kusema ni, “Suruali za zamani msizitupe, mtazihitaji baadae,” na “Watakaobaki  Dar es Salaam baada ya mwezi wa saba watakuwa wanaume kwelikweli.”

Dk Abbasi amesema walipotakiwa kuthibitisha wapi iwe ndani au nje ya nchi Rais alipata kutoa kauli hizo, wahariri wa Raia Mwema waliomba muda ambao walipewa. “Wakarejea na kuthibitisha kuwa hawana ushahidi huo, wakakiri kosa na kuomba radhi.”

Mkurugenzi huyo amesema bado Serikali inaamini Watanzania wakiufanyia mzaha upotoshaji wa taarifa na uchochezi katika zama hizi za Tehama amani na utulivu uliopo kwa miaka mingi utapotea na kukaribisha maafa kama ilivyotokea kwingineko duniani.

“Serikali, katika uamuzi huu, uliochukuliwa kwa mujibu wa mamlaka aliyonayo Waziri wa Habari katika kifungu cha 59 cha Sheria ya Huduma za Habari Na. 12, 2016, imetoa adhabu ndogo tofauti na ukubwa wa kosa kwa kuwa wahariri wa gazeti hili hawakufanya tashtiti, wamekiri kosa,” amesema.

Dk Abbasi amesema kupitia hilo, wamejifunza mambo kadhaa kuhusu changamoto za kiwango cha weledi wa uandishi wa habari nchini kiasi cha kuwalazimu kutoa ufafanuzi wa kina kwa faida ya umma na tasnia yenyewe; kwamba uandishi ni taaluma adhimu na yenye haki na wajibu vinavyopaswa kufuatwa na si kufanyiwa dhihaka.

Share:

Amuua mwenzake kisa mabishano kuhusu makalio ya mwanamke


Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani Kamishna Msaizidizi Jonathan Shanna Warioba, ametoa onyo kali kwa wananchi wenye tabia za udhalilishaji kwa wanawake kuacha tabia hiyo mara moja huku akisema kwamba udhalilishaji umesababisha kifo.

Kamanda Shanna amelazimika kusema hayo  hayo wakati akitolea ufafanuzi juu ya tukio la mauaji ya mkazi wa Kijiji  cha Vilabwa Wilaya ya Kisarawe Imma Habibu ( 26).

Kwa mujibu wa Shanna Marehemu aliuwawa juzi majira ya saa mbili asubuhi wakati walipokuwa kijiweni na wenzake baada ya kutokea ugomvi kati yake na Ramadhani Habibu (23) ambaye ni ndugu yake, baada ya mwanamke mmoja ambaye anadaiwa kuwa na maumbile makubwa (makalio) kupita, mbele yao.

Alisema baada ya mwanamke huyo kupita mbele yao walianza mabishano ambapo marehemu alisema mwanamke huyo ana makalio makubwa na Ramadhani alisema ni makalio ya kawaida sio  makubwa.

Kamanda Shanna alieleza kuwa baada ya mabishano hayo ndipo ulipozuka ugomvi hadi kufikia hatua ya Ramadhani kumuua kaka yake kwa kumchoma kisu kifuani upande wa kuliana na alifariki dunia akiwa njiani anapelekwa hosptali ya kisarawe.

Alisema jeshi la polisi linamshikilia mtuhumiwa kwa kufanya mauaji hayo na kuwa atafikishwa mahakamani mara moja  na kuwa amekubali kuwa amefanya mauaji hayo.

Kufuatia,tukio hilo kamanda Shanna aliendelea kutoa onyo kwa wananchi na  vijana wanaoshinda vijiweni kuacha tabia ya udhalilishaji hasa kwa wanawake na kuwa  kufanya hivyo ni kosa kisheria na kuwa kama kuna mtu aliyefanyiwa vitendo vya namna hiyo atoe taarifa polisi na atafikishwa mahakamani.

"Wito kwa wale wanaokiuka haki za binadamu kwa kumdhalilisha mtu waache mara moja, mfano kisheria hata kumkonyeza mtu ni kosa la jinai hivyo unapaswa kufika polisi, na tutamfuatilia kisha kumpeleka mahakamani" Kamanda Shana amefafanua

Pia kamanda Shanna ametoa rai kwa wanawake kuvaa nguo zinazositiri maungo yao ili kuepusha vishawishi na matamanio kwa wanaume
Share:

Total Pageviews

MC ELLY NGWALA

FOR BOOKING PLEASE CALL Business No: +255 713 404 646 +255 784 297 582 +255 767 404 647 Email: mcellyngwala@yahoo.com

MC ELLY NGWALA KTK POZI

My Blog List

Powered by Blogger.