Friday, 29 September 2017

Serikali yalifungia gazeti la Raia Mwema


Serikali imesitisha uchapishaji na usambazaji wa gazeti la kila wiki la Raia Mwema kwa muda wa siku 90 kuanzia leo.

Mkurugenzi wa Idara ya Habari (Maelezo) na Msemaji Mkuu wa Serikali, Dk Hassan Abbasi amesema leo Alhamisi kuwa agizo hilo pia linahusu toleo la mtandaoni.

Dk Abbasi amesema adhabu hiyo inatokana na toleo namba 529 la Septemba 27 hadi  Oktoba 3 lililochapisha habari ya uchambuzi inayosomeka “Urais utamshinda John  Magufuli.”

Mwenyekiti wa Bodi ya Raia Mwema, Jenerali Ulimwengu amesema wameambiwa sababu ya kusitishwa kwa gazeti hilo ni habari hiyo.

Ulimwengu amesema kwa sasa wanashauriana kuona ni nini cha kufanya.

Dk Abbasi amesema katika taarifa kwa vyombo vya habari kuwa, Serikali inasisitiza uchambuzi huo ni maoni ya Raia Mwema  ya haki (fair comment), hata hivyo, kwa bahati mbaya, na nia ovu, makala hiyo ilisheheni nukuu za kutunga na zisizo za kweli zikimsingizia Rais John Magufuli.

Amesema gazeti hilo pia limewahi kuonywa kwa makosa mbalimbali.

Amesema nukuu za uongo, kutungwa na zenye nia mbaya zikidai Rais alipata kusema ni, “Suruali za zamani msizitupe, mtazihitaji baadae,” na “Watakaobaki  Dar es Salaam baada ya mwezi wa saba watakuwa wanaume kwelikweli.”

Dk Abbasi amesema walipotakiwa kuthibitisha wapi iwe ndani au nje ya nchi Rais alipata kutoa kauli hizo, wahariri wa Raia Mwema waliomba muda ambao walipewa. “Wakarejea na kuthibitisha kuwa hawana ushahidi huo, wakakiri kosa na kuomba radhi.”

Mkurugenzi huyo amesema bado Serikali inaamini Watanzania wakiufanyia mzaha upotoshaji wa taarifa na uchochezi katika zama hizi za Tehama amani na utulivu uliopo kwa miaka mingi utapotea na kukaribisha maafa kama ilivyotokea kwingineko duniani.

“Serikali, katika uamuzi huu, uliochukuliwa kwa mujibu wa mamlaka aliyonayo Waziri wa Habari katika kifungu cha 59 cha Sheria ya Huduma za Habari Na. 12, 2016, imetoa adhabu ndogo tofauti na ukubwa wa kosa kwa kuwa wahariri wa gazeti hili hawakufanya tashtiti, wamekiri kosa,” amesema.

Dk Abbasi amesema kupitia hilo, wamejifunza mambo kadhaa kuhusu changamoto za kiwango cha weledi wa uandishi wa habari nchini kiasi cha kuwalazimu kutoa ufafanuzi wa kina kwa faida ya umma na tasnia yenyewe; kwamba uandishi ni taaluma adhimu na yenye haki na wajibu vinavyopaswa kufuatwa na si kufanyiwa dhihaka.

Share:

0 comments:

Post a Comment

Total Pageviews

MC ELLY NGWALA

FOR BOOKING PLEASE CALL Business No: +255 713 404 646 +255 784 297 582 +255 767 404 647 Email: mcellyngwala@yahoo.com

MC ELLY NGWALA KTK POZI

My Blog List

Powered by Blogger.