Wednesday, 27 September 2017

Waziri Mkuu atoa maagizo kwa Wakuu wa Mikoa 11

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewataka wakuu wa mikoa 11 inayolima pamba nchini wahakikishe wanasimamia vizuri wakulima wa zao hilo ili kuongeza uzalishaji na kuwaletea tija wananchi.

Agizo hilo limetolewa Jumanne, Septemba 26, 2017 na Waziri Mkuu wakati akizungumza na wakuu hao wa mikoa kwenye kikao alichokitiisha mjini Dar es Salaam kujadili maendeleo ya zao hilo.

Kikao hicho ni muendelezo wa kikao alichokitiisha mjini Dodoma (Ijumaa, Septemba 8, 2017) kujadili mbinu za kufufua zao hilo.

Wakuu wa mikoa walioitwa kwenye kikao hicho ni kutoka mikoa ya Shinyanga, Singida, Kagera, Tabora, Morogoro, Mara, Mwanza, Simiyu, Katavi, Kigoma na Geita.

Waziri Mkuu amesema katika kipindi hiki ambacho msimu wa maandalizi ya kilimo cha pamba umeanza ni vema kwa Maofisa Kilimo na Wagani wakawasimamia wakulima kwa ukaribu ili wahakikishe wanafuata mbinu bora za kilimo.

Amesema iwapo wakulima watapata usimamizi mzuri kutoka kwa Maofisa Ugani waliopo kwenye maeneo yao kuanzia hatua za awali za utayarishaji wa mashamba yao itawasaidia katika kuongeza tija, kwenye uzalishaji wao.

“Serikali inawataka Maofisa Kilimo na Wagani wawasimamie wakulima kuanzia maandalizi ya shamba, kupanda, matumizi ya pembejeo na dawa, kuvuna na kutafuta masoko ili kilimo cha zao hilo kiweze kuwaongezea tija.”

Amesema Maafisa Kilimo wote walioko kwenye kila Halmashauri ni lazima wahusike kikamilifu katika kuwaelekeza wakulima namna ya kutumia mbinu bora za kilimo ili waweze kupata mazao mengi , hivyo kujikwamua kiuchumi.

Pia Waziri Mkuu amewaagiza Wakuu wa Vyuo vya Kilimo nchini wahakikisha wanakuwa na mashamba darasa yatakayotumika na wakulima na wanafunzi wao kujifunza mbinu bora za kilimo kwa vitendo.

Kikao hicho kilihudhuriwa na Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Dkt. Charles Tizeba; Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – TAMISEMI; Bw. Suleiman Jafo, Makatibu Wakuu wa Ofisi ya Waziri Mkuu na Wizara ya Kilimo, Mrajis wa Vyama vya Ushirika nchini, Dkt. Tito Haule na Mkurugenzi Uhamasishaji Mazao, Bw. Twahir Nzallawahe.

IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU.
Share:

0 comments:

Post a Comment

Total Pageviews

MC ELLY NGWALA

FOR BOOKING PLEASE CALL Business No: +255 713 404 646 +255 784 297 582 +255 767 404 647 Email: mcellyngwala@yahoo.com

MC ELLY NGWALA KTK POZI

My Blog List

Powered by Blogger.