Mkazi wa Buguruni jijini
hapa, Deus Johakim Magosa (45) ambaye ni shahidi wa nane upande wa
Jamhuri katika kesi namba 303 ya mwaka 2016 ya kumjeruhi, kumtoboa macho
na kumfanyia unyang’anyi wa kutumia silaha, Saidi Mrisho inayomkabili
Salum Njwete ‘Scorpion’ katika Mahakama ya Wilaya ya Ilala jijini, leo
alinusurika kutupwa lupango baada ya Wakili Mwandamizi wa Serikali,
Nassoro Katuga kumtuhumu kutoa ushahidi wa uongo.
Wakili Katuga alimtuhumu
shahidi huyo kutokana na kutoa majibu tofauti wakati akimuongoza kutoa
ushahidi wake na maelezo aliyoyatoa awali Kituo cha Polisi cha
Buguruni.
Awali shahidi huyo
alisema mahakamani hapo kuwa hakuwahi kusikia popote kuwa Scorpion
amehusishwa katika tukio la kumshambulia Said, lakini baadaye alipobanwa
alisema ni kweli alisikia tetesi hizo kuwa mtuhumiwa huyo ndiye
aliyefanya tukio hilo. Pamoja na mambo mengine aliyomhoji na kumbaini
kuwa anatoa ushahidi wa uongo wakili Katuga
alipomgeukia hakimu
aliyekuwa akisikiliza kesi hiyo, Flora Haule na kumwambia shahidi
anazidi kuidanganya mahakama hiyo na kuitaka mahakama hiyo imchukulie
hatua kwa mujibu wa kifungu cha 164 cha ushahidi hapa nchini (Tanzania
Evidence Act).
Shahidi huyo alionekana
kuwa katika wakati mgumu baada ya wakili huyo kuwaita askari polisi na
kuwataka wakae tayari kumchukua shahidi huyo.
Hata hivyo kutokana na
ufinyu wa muda hakimu Flora aliahirisha kesi hiyo mpaka Aprili 18 mwaka
huu na kumuacha shahidi huyo aondoke na kumtaka kufika tena mahakamani
hapo tarehe iliyopangwa bila kukosa ambapo Scorpion naye alirudishwa
mahabusu mpaka tarehe hiyo.
Mwandishi wetu
alizungumza na mmoja wa wanasheria mahakamani hapo kuhusu ushahidi wa
uongo ambapo, mwanasheria huyo alisema unapobainika kutoa ushahidi wa
uongo ukiwa ndani ya kiapo unaweza kufungwa jela kati ya miezi sita
mpaka mwaka mmoja.
0 comments:
Post a Comment