Home »
BUNGENI
» HII HAPA Hotuba Ya Mhe. Waziri Mkuu Aliyoitoa Leo Bungeni
UTANGULIZI
- Mheshimiwa Spika, naomba kutoa Hoja kwamba kutokana
na taarifa zilizowasilishwa leo katika Bunge lako Tukufu na Mwenyekiti
wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria, Mwenyekiti wa Kamati
ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge
ya Masuala ya UKIMWI zilizochambua Bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu, Bunge
lako sasa lipokee na kujadili Taarifa ya Mapitio ya Utekelezaji wa Kazi
za Serikali kwa mwaka 2016/2017 na Mwelekeo wa Kazi za Serikali kwa
mwaka 2017/2018. Aidha, ninaliomba Bunge lako Tukufu likubali kupitisha
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha ya Ofisi ya Waziri Mkuu na
Taasisi zilizo chini yake pamoja na Mfuko wa Bunge kwa mwaka 2017/2018.
- Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2016/2017, Bunge
lako Tukufu limeondokewa na Wabunge wenzetu, Mheshimiwa Hafidh Ally
Tahir aliyekuwa Mbunge wa Jimbo la Dimani – CCM na Mheshimiwa Dkt. Elly
Marko Macha, aliyekuwa Mbunge wa Viti Maalum – CHADEMA. Pia, Taifa
lilimpoteza Mheshimiwa Samwel John Sitta aliyekuwa Spika Mstaafu wa
Bunge la Tisa la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Aidha, nchi yetu
imekumbwa na majanga na maafa yaliyosababisha vifo, majeruhi na
uharibifu wa mali. Ninaomba Mwenyezi Mungu awajalie nafuu ya haraka wale
wote waliopata majeraha, na kuwapumzisha kwa amani wale waliopoteza
maisha, Amina! Ninatoa pole kwa familia za wote waliopoteza ndugu, jamaa
na marafiki. Pia ninatoa pole kwa Mheshimiwa Aida Khenani aliyepata
ajali ya kugongwa na pikipiki wakati akitoka Bungeni. Tunamuombea apone
haraka na aweze kurejea Bungeni ili kuendelea na majukumu yake.
0 comments:
Post a Comment