Mkutano wa saba wa Bajeti wa Bunge la 11 unaanza leo mjini Dodoma
ambao Juni 15, mwaka huu utapokea taarifa ya hali ya uchumi na baadaye
jioni bajeti ya serikali kwa mwaka wa fedha 2017/2018.
Kwa mujibu wa ratiba iliyotolewa na Ofisi ya Bunge jana, Mkutano huo
wa Bunge la Bajeti utamalizika Juni 30, mwaka huu, na kwa kuanzia leo,
utafanya kazi ya kumwapisha Mbunge wa Kuteuliwa, Mama Salma Kikwete na
kisha kuwachagua wabunge tisa wa kuiwakilisha Tanzania katika Bunge la
Afrika Mashariki (EALA).
Aidha, kutakuwa na majumuisho kati ya serikali na Kamati ya Bajeti.
Kesho Bunge mbali ya Kipindi cha Maswali na Majibu, pia serikali na
Kamati ya Bajeti wataendelea na mashauriano na baadaye Kamati ya Uongozi
itapokea taarifa ya Kamati ya Bajeti na Mashauriano ya Serikali.
Ratiba hiyo inaonesha kuwa bajeti za kisekta zitaanza Alhamisi wiki
hii, kwa Ofisi ya Waziri Mkuu kuwasilisha, ambapo baada ya kuwasilishwa
itajadiliwa kwa siku tano hadi Aprili 13, mwaka huu kabla ya Bunge
kuingia katika mapumziko ya Ijumaa Kuu, Jumapili ya Pasaka na Jumatatu
ya Pasaka.
Baada ya mapumziko hayo, Ofisi ya Rais ambayo ina wizara mbili za
Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na Menejimenti ya Utumishi wa Umma
na Utawala Bora itawasilisha bajeti yake Aprili 18 ambayo itajadiliwa
hadi Aprili 21, mwaka huu.
Ofisi ya Makamu wa Rais zamu yake itakuwa Aprili 24 ikihusisha
masuala ya Muungano na Mazingira, na siku inayofuata itakuwa zamu ya
Bajeti ya Wizara ya Katiba na Sheria itakayofuatiwa na Wizara ya Ujenzi,
Uchukuzi na Mawasiliano baada ya Sikukuu ya Muungano, na itaendelea
baada ya Sikukuu ya Mei Mosi.
Mei 3, itakuwa zamu ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia,
Wazee na Watoto kwa siku mbili, kisha Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa
na Michezo kwa siku mbili, Mei 5 na Mei 8, mwaka huu, kabla ya Wizara
ya Mambo ya Ndani ya Nchi itakuwa Mei 9, mwaka huu kwa siku moja.
Bajeti zitakazofuata baada ya hapo kwa mtiririko ni Maji na
Umwagiliaji, Elimu, Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi; Ulinzi na
Jeshi la Kujenga Taifa; Viwanda, Biashara na Uwekezaji; Kilimo, Mifugo
na Uvuvi; Maliasili na Utalii; Nishati na Madini; Ardhi, Nyumba na
Maendeleo ya Makazi; Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki na
Fedha na Mipango itakamilisha bajeti za kisekta Juni 5 na 6, mwaka huu.
Kuanzia Juni 7 hadi 9, mwaka huu, serikali kwa kushauriana na Kamati
ya Bajeti watafanya majumuisho kuzingatia hoja zenye maslahi kwa Taifa
zilizojitokeza wakati wa kujadili Bajeti za Wizara; kabla ya Dk Philip
Mpango kuwasilisha Taarifa ya Hali ya Uchumi na Bajeti ya Serikali, Juni
15, mwaka huu. Bajeti itajadiliwa kwa siku saba kuanzia Juni 17 hadi
Juni 24, mwaka huu itakapopitishwa kwa kura za wabunge.
0 comments:
Post a Comment