Katika
kusherekea siku ya Maulid ya kuzaliwa Mtume Muhammed (S.A.W), Waziri
Mkuu, Kassim Majaliwa amesema kuwa Serikali itaendelea kuwatumikia
Watanzania wote bila kujali imani zao za kidini.
Majaliwa
ameyasema hayo katika sherehe za kitaifa za Maulid ambazo zimefanyika
mkoani Singida na kusema kuwa kuna matukio ambayo yamekuwa yakijitokeza
katika jamii na katika kuyachukulia hatua za kisheria vitendo hivyo
Serikali haitakuwa ikibagua mtu kutokana na imani yake ya kidini kama
jinsi inavyofanya kwa shughuli za maendeleo.
“Serikali
inawashukuru sana kwa kuendelea kuunga mkono jitihada ya Serikali ya
Rais Magufuli, tunaamini juhudi tunazofanya za kuweka nidhamu kwa
watumishi wa umma na taasisi binafsi mtaendelea kutuunga mkono,
tutaendelea kuruhusu uhuru wa kuabudu na kushirikiana na viongozi wa
dini lakini tu mafundisho yanayotolewa yasikiuke sheria na kanuni za
nchi,
“Serikali
ipo macho kupambana na tukio lolote lenye nia ya kupoteza amani ya nchi
yetu, Watanzania tushirikiane kutoa taarifa ili hatua zichukuliwe, ni
vyema mtambue ninyi kama viongozi na waumini ndiyo walinzi wa nchi yetu,
niwambie tu kuwa Serikali itaendelea kuwatumikia Watanzania wote bila
kujali dini ya mtu wala kabila,” amesema Majaliwa.
Nae Mufti Mkuu wa Tanzania, Sheikh Abubakar Zubeiry amesema
“Jambo ambalo Waislamu tunatakiwa kuwa nayo ni kupendana, tufanye kama
Mtume wetu, yeye alikuwa akijenga mshikamano, akijenga upendo akijenga
umoja na kama tunataka kumfata tumwige Mtume katika kupendana, tuache
majungu, fitna na tuache kila kitu kisicho na faida,
“Kwanini
mnagombana Waislamu na nyie ni watu wa Mungu, Waislamu tuwe na
mshikamano kama tuliokuwa nao, pia tunao undugu wa Tanzania, tupendane
kama Watanzania na mwenyezi Mungu ametwambia tusibague hata kama sio
Waislamu, Mungu hakatazi mtu kumtendea wema mtu mwingine kama tu
hakufanyi mabaya na hayo ndiyo mafunzo ya Uislamu.”
0 comments:
Post a Comment