Monday 12 December 2016

Sherehe za Maulid: Waziri Mkuu Asema Serikali itaendelea kuwatumikia Watanzania wote bila kujali dini Zao

Katika kusherekea siku ya Maulid ya kuzaliwa Mtume Muhammed (S.A.W), Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amesema kuwa Serikali itaendelea kuwatumikia Watanzania wote bila kujali imani zao za kidini.

Majaliwa ameyasema hayo katika sherehe za kitaifa za Maulid ambazo zimefanyika mkoani Singida na kusema kuwa kuna matukio ambayo yamekuwa yakijitokeza katika jamii na katika kuyachukulia hatua za kisheria vitendo hivyo Serikali haitakuwa ikibagua mtu kutokana na imani yake ya kidini kama jinsi inavyofanya kwa shughuli za maendeleo.

“Serikali inawashukuru sana kwa kuendelea kuunga mkono jitihada ya Serikali ya Rais Magufuli, tunaamini juhudi tunazofanya za kuweka nidhamu kwa watumishi wa umma na taasisi binafsi mtaendelea kutuunga mkono, tutaendelea kuruhusu uhuru wa kuabudu na kushirikiana na viongozi wa dini lakini tu mafundisho yanayotolewa yasikiuke sheria na kanuni za nchi,

“Serikali ipo macho kupambana na tukio lolote lenye nia ya kupoteza amani ya nchi yetu, Watanzania tushirikiane kutoa taarifa ili hatua zichukuliwe, ni vyema mtambue ninyi kama viongozi na waumini ndiyo walinzi wa nchi yetu, niwambie tu kuwa Serikali itaendelea kuwatumikia Watanzania wote bila kujali dini ya mtu wala kabila,” amesema Majaliwa.

Nae Mufti Mkuu wa Tanzania, Sheikh Abubakar Zubeiry amesema “Jambo ambalo Waislamu tunatakiwa kuwa nayo ni kupendana, tufanye kama Mtume wetu, yeye alikuwa akijenga mshikamano, akijenga upendo akijenga umoja na kama tunataka kumfata tumwige Mtume katika kupendana, tuache majungu, fitna na tuache kila kitu kisicho na faida,

“Kwanini mnagombana Waislamu na nyie ni watu wa Mungu, Waislamu tuwe na mshikamano kama tuliokuwa nao, pia tunao undugu wa Tanzania, tupendane kama Watanzania na mwenyezi Mungu ametwambia tusibague hata kama sio Waislamu, Mungu hakatazi mtu kumtendea wema mtu mwingine kama tu hakufanyi mabaya na hayo ndiyo mafunzo ya Uislamu.”
Share:

0 comments:

Post a Comment

Total Pageviews

MC ELLY NGWALA

FOR BOOKING PLEASE CALL Business No: +255 713 404 646 +255 784 297 582 +255 767 404 647 Email: mcellyngwala@yahoo.com

MC ELLY NGWALA KTK POZI

My Blog List

Powered by Blogger.