Mahakama
ya Hakimu Mkazi Kisutu imemuachia huru mke wa marehemu bilionea Erasto
Msuya, Miriam Mrita na mwenzake Revocatus Muyela wanaokabiliwa na kesi
ya mauaji ya Aneth Msuya.
Hata hivyo washtakiwa hao walikamatwa tena na jeshi la polisi.
Hakimu
Mkazi Mkuu, Godfrey Mwambapa leo amewaachia huru washtakiwa hao baada
ya upande wa mashtaka kushindwa kutimiza amri yake iliyowataka kufanyia
marekebisho ya hati ya mashtaka
Washtakiwa hao walikuwa wanakabiliwa na kesi ya mauaji ya kukusudia.
Uamuzi
wa mahakama kuifuta kesi hiyo umefikiwa leo baada ya jalada la kesi
hiyo lililokuwa limeitwa Mahakama Kuu kurejeshwa mahakamani hapo.
Februari 20, mwaka huu, Hakimu Mwambapa aliupatia upande wa mashtaka muda wa siku tatu kurekebisha hati ya mashtaka.
Lakini
mpaka siku hizo tatu zinaisha hawakuwa wamefanyia bali Wakili wa
Serikali, Hellen Moshi aliiambia mahakama kuwa baada ya ofisi yao
kutafakari kwa kina wameamua kuwa hawana cha kubadilisha kwa hati hiyo
ya mashtaka
Wakili
wa utetezi, Peter Kibatala alidai kuwa upande wa mashtaka licha ya
kupewa muda wa kutosha kufanyia marekebisho hati hiyo lakini wamekaidi
amri hiyo.
Kibatala
aliiomba mahakama kuwaachia washtakiwa huru kwa kuwa amri ya mwisho ya
mahakama ilisema kama wasipofanya marekebisho itachukua hatua na pia
hakuna rufaa yoyote iliyokatwa na Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) kupinga
uamuzi huo.
Hakimu
Mwambapa amesema,kweli mahakama imeamuru upande wa mashtaka kufanyia
marekebisho hati ya mashtaka pindi ilipoona inamapungufu lakini
hawakufanya hivyo, akawaongezea muda hawakufanya hivyo, Ila leo wamekuja
na maelezo ya kuwa hati ya mashtaka ni sahihi.
"Hati ipi ambayo ipo sahihi wakati mahakama ilisema haipo sahihi, nawaachia huru washtakiwa", amesema Mwambapa.
Awali
ndugu wa marehemu waliwasilisha barua mahakamani hapo na Kwa mujibu wa
barua hiyo walikuwa wanataka Hakimu huyo ajitoe kwa sababu hawana imani
naye.
Hakimu
Mwambapa alikuwa atoe uamuzi juu ya hoja zilizowasilishwa na upande wa
utetezi pamoja na upande wa mashtaka ambapo Wakili John Malya aliomba
washtakiwa hao waachiwe huru kwa sababu hakuna hati ya mashtaka
inayowashikilia washtakiwa hao mahakamani hapo.
Wakili
wa Serikali Mwandamizi, Kishenyi Mutalemwa yeye aliiomba mahakama iwape
muda ili waweze kutekeleza amri ya mahakama iliyotolewa Januari 9,
mwaka huu
Washtakiwa
Miriam na Revocutus wanadaiwa kumuua kwa makusudi Aneth Msuya, kwa
kumchinja, nyumbani kwake Kigamboni jijini Dar es Salaam.
Miriam
ambaye ni mshtakiwa wa kwanza katika kesi hiyo alikuwa mke wa aliyekuwa
kaka wa Aneth, marehemu Erasto Msuya, maarufu kama bilionea Msuya.
Erasto
Msuya, ambaye alikuwa mfanyabiashara bilionea wa madini ya Tanzanite,
pia aliuawa kwa kupigwa risasi, Agosti, 2015 eneo la Mijohoroni, kando
ya barabara ya Arusha – Moshi wilayani Hai mkoani Kilimanjaro.
Hata hivyo washtakiwa hao walikamatwa tena na kuondoka na gari la polisi.
0 comments:
Post a Comment