Waziri
Mkuu Kassim Majaliwa amepokea taarifa rasmi ya uchunguzi wa kifo cha
Faru John kutoka kwa Mkemia Mkuu wa Serikali, Prof. Samwel Manyele
ambaye alikuwa akiongoza tume maalum iliyoundwa na Waziri Mkuu.
Akisoma
taarifa hiyo mbele ya Waziri Mkuu, Prof. Manyele amesema tume yake
ilifanya uchunguzi wa kifo cha Faru John kwa kupima vinasaba vya sampuli
mbalimbali vikiwemo mzoga, fuvu, mifupa, pembe, damu, ngozi na kinyesi
kilichokaushwa ambapo ilibainika kuwa vyote ni vya mnyama mmoja, aina ya
faru mweusi ambaye ni dume.
Prof.
Manyele amesema matokeo hayo yamethibitisha kuwa faru John alikufa
katika hifadhi ya Sasakwa Grumeti kwa kukosa matunzo na uangalizi wa
karibu.
“Maabara
iliyotumika ni ya Chuo Kikuu cha Pretoria, Afrika Kusini chini ya
usimamizi wa timu ya wataalamu kutoka Tanzania, wachunguzi wa Serikali,
chini ya Ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali. Sababu za kifo chake
zilichangiwa na kukosa matunzo na uangalizi wa karibu, kukosa matibabu
alipoumwa, mazoea yanayotokana na kutofuata taratibu zilizowekwa
kisheria na mapungufu ya kiuongozu kwa Wizara husika, hifadhi na taasisi
zake,” amesema.
Prof.
Manyele amesema mapungufu waliyoyabaini kutokana na uchunguzi huo ni
kutokuwepo kwa kibali rasmi cha kumhamisha Faru John; kukosekana kwa
mkataba wa kupokelewa kwa Faru John hifadhi ya Sasakwa Grumeti na
kutofuatiliwa kwa afya na maendeleo ya Faru John baada ya kuhamishwa.
Mengine
ni uchukuaji holela wa sampuli za wanyama pori kwa lengo la utafiti na
kuzisafirisha nje ya nchi; migongano ya kimaslahi kati ya watumishi
waliolenga kusimamia taratibu na wale wenye kusimamia maslahi binafsi na
uwepo wa taasisi nyingi zenye mamlaka sawa juu ya masuala ya uhifadhi
wa wanyamapori.
“Pamoja
na kwamba mawasiliano yanaonyesha zoezi hilo liliridhiwa na Wizara,
hapakuwepo na kibali rasmi kutoka kwa Mkurugenzi wa Wanyamapori cha
kuruhusu kumhamisha Faru John kutoka NCAA kwenda Grumeti,” amesema Prof.
Manyele katika ripoti yake.
Kwa
upande wake Waziri Mkuu ameishukuru timu ya uchunguzi iliyokuwa chini
ya Mkemia Mkuu wa Serikali kwa kazi iliyoifanya ikiwemo kuainisha
udhaifu uliokuwemo ndani ya Wizara ya Maliasili na Utalii na taasisi
zake.
“Ofisi
yangu itaipitia taarifa hii ambayo ni kubwa kiasi na kuifanyia kazi.
Matokeo ya kazi hiyo, tutayatoa hivi karibuni ili kuonyesha Serikali
imeamua kufanya nini juu ya mapendekezo yaliyotolewa.”
Amemtaka
mkurugenzi Msaidizi wa Kitengo cha Kupambana na Ujangili wa
Wanyamapori, Bw. Robert Mande, afuatilie mapendekezo yaliyoainishwa na
tume hiyo na wayafanyie kazi mapema iwezekanavyo
0 comments:
Post a Comment