KATONI 32,634 za pombe kali zilizofungashwa kwenye vifungashio vya
plastiki (viroba) zenye thamani ya zaidi ya Sh bilioni 5.18 zimekamatwa
jana, katika operesheni maalumu ya utekelezaji wa maelekezo ya Serikali
ya kusitisha uzalishaji, usambazaji, uingizaji, uuzaji na matumizi ya
pombe hizo.
Pombe hizo zimekamatwa katika operesheni inayoendelea katika mikoa
mitatu ya Kikodi ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Dar es Salaam
ambayo ni Temeke, Kinondoni na Ilala.
Akizungumza katika operesheni hiyo, Mkaguzi kutoka Mamlaka ya Chakula na
Dawa (TFDA), John Nzila alisema walikamata katoni 14,393 za konyagi,
katoni 9,964 za Vradmill, Zanzi 31 na Valeur. 268.
Alisema mzigo huo ulikutwa katika ghala la Loverira Enterprises lililopo
Kimara Temboni na kwamba mzigo huo umezuiwa kwa hatua zaidi.
Kwa upande wake Mwanasheria Mwandamizi wa Baraza la Taifa la Hifadhi na
Usimamizi wa Mazingira (NEMC), Heche Suguta alisema kuwa walikamata
katoni 7,000 za viroba vya aina mbalimbali zikiwemo Konyagi, Zanzi
pamoja na Burudani vyote vikiwa na thamani zaidi ya Sh bilioni 2.
Alisema vinywaji hivyo vilikutwa katika duka la Love Kira Enterprises
lililopo Wazo na kwamba mzigo huo umezuiwa hadi utaratibu mwingine
utakapotangazwa.
Kwa upande wa Temeke yalikamatwa maboksi matano ya Konyagi, maboksi 15
ya Black Bee, maboksi nane ya Zanzi na Maboksi matano ya Valeur.
Ofisa Afya wa Manispaa ya Temeke ambaye pia ni mratibu wa Masuala ya
Chakula katika Manispaa hiyo, Rehema Sadick alisema katika operesheni
hiyo wamegundua kwamba wafanyabiashara wengi hawana vibali vya TFDA na
leseni za biashara.
Hata hivyo katika operesheni hiyo pia kulibainika kuna baadhi ya
wafanyabiashara wanauza vileo vilivyokwisha muda wake na hivyo
kuvikamata kwa ajili ya kuokoa afya za watumiaji.
0 comments:
Post a Comment